Mwimbaji, mtunzi na mtumbuizaji wa nyimbo za mahadhi ya Taarabu, Mzee Yusuf anatimiza miaka 20 tangu aingie kwenye tasnia hii akiwa kijana kabisa. Mzee Yusuf mzaliwa wa visiwa vya Zanzibar alijipatia umaarufu kama mfalme wa muziki wa kizazi kipya cha Taarabu yaani ‘Modern Taarab’. Hii ni kwasababu hapo awali muziki wa Taarabu ulikuwa wa taratibu usio na midundo ya kucheza kama ilivyo sasa, na moja ya waasisi wa muziki wa Taarabu ya kizazi kipya ni Mzee Yusuph.
Aliwahi kuulizwa hapo nyuma safari yake ya muziki ilipoanzia na alielezea kwa kina namna alivyoanza. Mzee Yusuph alianza safari yake ya muziki huko Zanzibar akiwa bado anasoma, na baada ya muda aliona aache shule ili ajikite zaidi katika uimbaji na hii ilitokana na ugumu wa maisha kwa kipindi hiko, lakini pia ilhali anaimba alijiingiza kwenye sanaa ya maigizo na hapo akajizolea umarufu hadi kuchukuliwa na bendi ili awe mmoja ya wasanii wao.
Muziki wa Taarabu kwa Zanzibar ndio aina ya muziki unaopendwa zaidi na ilikuwa rahisi kwa Mzee Yusuf kuvutiwa nao ukijumlisha na uwezo wake wa kuimba, ikawa rahisi kwake kuanza na kuendelea kuwa bora zaidi kadiri siku zilivyokuwa zinaenda. Mzee Yusuph pia alidokeza kuwa mama yake mzazi pia alikuwa mwanamuziki wa Taarabu, hii nayo ni sababu nyingine kubwa iliyomvutia na yeye kufanya muziki wa aina hiyo.
Mzee Yusuf Mwinyi ndio jina lake kamili na katika familia yao yupo na dada yake anayejulikana kwa jina la Khadija Yusuph ambaye nae pia ni mwimbaji maarufu wa muziki wa Taarabu. Mzee Yusuf anaejulikana kama King of Modern Taarab alianzisha kundi ama bendi yake ya Taarabu iliyojulikana kama Zanzibar Modern Taarab mnamo mwaka 2001 na baada ya miaka kadhaa aliibadili jina na kuiita Jahazi Modern Taarab.
Kupitia bendi yake amekuza vipaji vya wasanii kadhaa ambao hadi miaka hii na wao wamekuwa wasanii wakubwa kwenye tasnia ya muziki hususani wa Taarabu, mmoja ya wasanii hao ni Bi. Isha Mashauzi ambaye alipita katika mikono ya fundi Mzee Yusuph na sasa ni moja ya wasanii wenye mafanikio kwa kufanya muziki wa Taarabu.
Ukiachana na kuimba na kutumbuiza, yeye pia ni mtunzi mzuri wa nyimbo ambazo zimeimbwa na wasanii wengine haswa wa kwenye bendi yake ya Jahazi, baadhi ya nyimbo maarufu ni pamoja na “Sina muda huo”, “Hakuna mkamilifu”, “Nilijua mtasema” na nyingine nyingi. Nyimbo zake maarufu alizoimba mwenyewe ni pamoja na "Kipendacho Roho," "Nitadumu Nae," and "Mpenzi Chocolate."
Mwaka 2017 Mzee Yusuf alitangaza kuachana na muziki wa Taarabu ili kufuata imani yake ya kidini, kwa mujibu wake haikuwa sawa na baada ya kutoka kuhiji Macca alilazimika kuweka pembeni utumbuizaji na uimbaji na bendi yake iliendelea bila yeye kufanya nao muziki. Baada ya miaka mitatu ama minne mbele alirejea kwa upya katika tasnia na ameweza kuachia nyimbo nyingi zaidi lakini pia matamasha yake ambayo yalijizolea umaarufu kipindi cha nyuma ameyarejesha tena na wapenzi wa muziki wake wanafurahia uwepo wake.
Ukiachana na uimbaji Mzee Yusuf ameonekana kwenye filamu chache za bongo movie akionesha kipaji chake kingine cha kuigiza, na ni wazi ni mtu mwenye vipawa vingi ambavyo anavitumia kuendesha maisha yake
Tunampongeza kwa kuwa chachu ya burudani nzuri ya muziki, na ni moja kati ya watu muhimu kwenye tasnia ya muziki wa Taarabu, ni muhimu apewe maua yake kwa kuwa kazi aliyoifanya na anayoendelea kuifanya inasadiki jitihada na kujitoa kwake kwa wapenzi wa muziki mzuri, hakika mfalme tunae na tunatamba nae.
Share hapo chini nyimbo zako pendwa kutoka kwa Mzee Yusuph iwe alizoimba yeye au alitunga na ukaburudika nayo.
Comments